
Na Mwandishi Wetu
WADAU
wa teknolojia na usimamizi wa intaneti wametakiwa kutumia fursa
zinazotokana na mtandao huo kwa maendeleo ya jamii badala ya kuutumia
kwa matusi, chuki, udhalilishaji na vitendo vinavyoweza kuathiri maslahi
na haki za watu wengine.
Rai hiyo imetolewa na
Mratibu wa Tanzania Internet Governance Forum (TIGF), Dkt. Nazarius
Kirama, wakati wa Mkutano wa 13 wa Jukwaa la Usimamizi wa Intaneti
Tanzania, unaojadili masuala mbalimbali yanayohusu matumizi, usalama na
mustakabali wa intaneti nchini.
Kirama amesema
mkutano huo umewakutanisha wadau kutoka serikalini, mashirika yasiyo ya
kiserikali, sekta binafsi, wataalamu na wasomi kutoka vyuo vikuu kwa
lengo la kujadili namna ya kukuza matumizi salama na yenye tija ya
intaneti, huku masuala ya akili mnemba (AI), ujumuishi wa kidijitali,
ulinzi wa taarifa binafsi na intaneti yenye kasi yakiwa miongoni mwa
mada zinazojadiliwa.
Amesema Jukwaa la
Usimamizi wa Intaneti Tanzania lilianza mwaka 2005 na ni sehemu ya mfumo
wa mijadala ya usimamizi wa intaneti unaofanyika katika ngazi za
kitaifa, kikanda na kimataifa, uliolenga kutoa nafasi kwa wadau kujadili
namna bora ya kusimamia mustakabali wa teknolojia hiyo.
Kirama
amesema licha ya intaneti kuwa nyenzo muhimu ya kufikisha huduma,
taarifa na fursa kwa watu wengi, baadhi ya watumiaji wamekuwa wakiitumia
vibaya kwa kutoa lugha za matusi, chuki na vitendo vinavyoweza kuharibu
maslahi ya wengine, akisema tabia hizo zinaakisi changamoto zilizopo
katika jamii.
“Jamii iliyopo kwenye mitandao ya
kijamii haikutoka mbinguni, inatokana na jamii yetu. Kwa hiyo yale
mambo yanayofanyika mtaani yanaweza pia kufanyika mtandaoni,” amesema
Kirama, huku akiwataka watumiaji kujenga utamaduni wa kujidhibiti badala
ya kutegemea udhibiti wa mamlaka pekee.
Amesema
wananchi wanapaswa kutafakari thamani wanayoipata kutokana na matumizi
ya intaneti na kuhakikisha fedha wanazolipia huduma hiyo zinatumika kwa
shughuli zenye manufaa, ikiwamo kujenga jamii, kuelimisha, kuongeza
fursa za kiuchumi na kuunganisha watu. “Intaneti ya bure bila faida ni
kujiletea umaskini.
Kwa nini utumie fedha kulipia intaneti halafu uitumie kumtukana mtu? Intaneti yenyewe ina gharama,” amesema.
Katika
mkutano huo, Mwanaharakati wa masuala ya teknolojia na miundombinu ya
TEHAMA, Damilola Kihinde, amewataka wazazi, hospitali na wahusika
wengine wanaokusanya au kuhifadhi taarifa za watoto kuhakikisha taarifa
hizo zinalindwa ili kuepusha matumizi mabaya, udhalilishaji na uvunjwaji
wa haki zao za msingi.
Kihinde amesema mtoto
mdogo hawezi kufanya maamuzi kuhusu matumizi ya taarifa zake, hivyo
mzazi akiwa mlezi na mlinzi wake wa kwanza ana wajibu wa kuhakikisha
picha na taarifa zake hazishirikishwi au kutumiwa kwa namna inayoweza
kumletea madhara.
Amesema pia hospitali, ambazo
zinaweza kuwa wadhibiti wa taarifa kwa mujibu wa Sheria ya Ulinzi wa
Taarifa Binafsi, zinapaswa kuweka mifumo imara ya kulinda taarifa za
watoto na wagonjwa.
Amesisitiza kuwa ulinzi wa
taarifa binafsi za watoto ni jukumu la pamoja linalohitaji ushirikiano
wa wazazi, hospitali na wahusika wengine, huku maslahi bora ya mtoto na
haki yake ya faragha yakipewa kipaumbele.
Kwa
upande wake, Pious Sylvester, Mratibu wa Ushirikiano wa Shirika la
African Child Project, amesema jamii inapaswa kuongeza uelewa kuhusu
umuhimu wa kulinda taarifa za watoto, hasa katika kipindi ambacho
matumizi ya mitandao ya kijamii yanaendelea kuongezeka.
Amesema
Tanzania pia inapaswa kuendelea kushiriki katika majukwaa ya kikanda na
kimataifa kuhusu usimamizi wa intaneti ili kupata fursa ya kujadili
changamoto na kutoa mchango katika mijadala ya mustakabali wa
teknolojia.
0 Comments