Na Kareny Masasy,Kahama
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita amekabidhi hundi ya zaidi ya shilingi bilioni 2.167 kwa vikundi 96 vya vijana ,wanawake na watu wenye ulemavu Manispaa ya Kahana huku makundi ya vijana waliofanikiwa kupata mikopo watumie kwa malengo.
Mhita ametoa kauli hiyo leo wakati wa hafla ya kukabidhi hundi hiyo ya fedha iliyotokana na mapato ya ndani ya asilimia kumi nakupatiwa vikundi 96 vinavyojishughulisha na ujasiliamali wa aina tofauti tofauti.
Mhita amesema mikopo hiyo inapaswa kuwa chachu ya kukuza shughuli za kiuchumi, kuongeza ajira na kuboresha maisha ya wanufaika hivyo ni muhimu kwa vikundi vilivyopatiwa fedha hizo kuhakikisha vinazitumia kwa uaminifu na uwajibikaji nasio katika anasa au kuweka heshima baa.
"Kumbukeni fedha hizi ni mikopo inayopaswa kurejeshwa kwa wakati ili kutoa fursa kwa vikundi vingine kunufaika na mpango huo kwani inalenga kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupata mitaji" Aliongeza Mhita.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama Masudi Kibetu akitoa taarifa juu ya mikopo hiyo amesema tangu kuanza kwa mpango huo mwaka 2025 hadi sasa, Manispaa imetoa mikopo zaidi ya Shilingi bilioni 6.377 kwa vikundi 335 vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Kabetu amesema katika robo ya kwanza na pili mwaka wa fedha 2026/2027 Manispaa imekabidhi Shilingi bilioni 2.167 kwa vikundi 96, ambapo vikundi 45 vya vijana vimepatiwa Shilingi bilioni 1.428, vikundi 46 vya wanawake Shilingi milioni 708.52 na vikundi vitano vya watu wenye ulemavu Shilingi milioni 31.
Kibetu amesema mikopo hiyo imewezesha vijana, wanawake na walemavu kupata guta za mizigo, bajaji na pikipiki za kusafirisha abiria, cherehani, kukuza biashara pamoja na kununua gari la kubeba samaki kutoka ziwani mpaka sokoni, hatua inayowafanya kupata fedha za kuendesha maisha.
Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Kaniki Mataluma amesema, mikopo hiyo inatokana na mapato ya ndani na inalenga kuwawezesha vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kujikwamua kiuchumi, kujitegemea na kuondokana na utegemezi wa kifamilia na mwaka ujao wa fedha wanatarajia kutoa zaidi ya Sh.bilioni 4.
Mmoja wa mjasiriamali mwenye ulemavu, Milaji Mrasi amesema kupata mkopo huo ni fursa muhimu kwake katika kuendeleza shughuli zake za ujasiriamali, kuongeza mtaji na kuboresha hali yake ya kiuchumi.
Milaji alipongeza serikali kwa kuanza kuwapatia mmoja mmoja tofauti na ilivyokuwa hapo awali kwani walipokuwa wakipata fedha waliishia kupigana badala ya kuwekeza kwenye biashara waliyokusudiwa na kuahidi kutumia mkopo alippata kujiinua kimaisha.
Abdallah Juma anayefanya kazi ya udereva wa bajaji amesema , mkopo huo utamsaidia kuimarisha shughuli zake za kiuchumi na kuongeza kipato ili kufikia malengo yake ya kimaisha ukilinganisha na alivyokuwa akiendesha bajaji ya mtu riba ilikuwa kubwa nakushindwa kufikia malengo.



0 Comments