VIJANA JIEPUSHENI NA VITENDO VYA UCHOCHEZI VINAVYOVURUGA AMANI


VIJANA  wametakiwa kujiepusha na vitendo vinavyochochea uvunjifu wa amani na kuacha kutumika  kwa maslahi ya watu wachache wanaolenga kuvuruga utulivu wa nchi badala yake wametakiwa kuwa walinzi wa amani, umoja na mshikamano pamoja na kukemea maovu katika jamii.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Mkoa wa Shinyanga (JMAT), Shehe Hamis Balilusa, wakati akizungumza katika mkutano wa Jeshi la Jadi Sungusungu uliofanyika  Kata ya Jana, Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga

Shehe Balilusa amesema amani ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa, akisisitiza kuwa bila kuwepo kwa amani hakuna shughuli za kijamii wala za kiuchumi zinazoweza kufanyika kwa ufanisi.

"Vijana ni nguvu ya taifa msikubali kutumika kuvuruga amani ya nchi badala yake, simameni kuilinda, kuimarisha umoja na kushirikiana na vyombo vya dola katika kukemea vitendo vya uhalifu," amesema

  Kamanda wa Jeshi la Jadi Sungusungu Mkoa wa Shinyanga, John Kadama amewataka Sungusungu kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi ili kuhakikisha haki inatendeka na wananchi wanaendelea kuwa na imani na jeshi hilo.

Amesema viongozi wa zamani wa sungusungu wanapochanguliwa walikuwa wanakwenda kuangalia sungusungu inaendaje lakini viongozi wa sasa wanapochaguliwa wanaanza kutunisha mabega hawataki kujua misingi ya sungusungu,tunasema hakuna kujichukulia sheria mkononi zingatieni sheria za nchi na kusimamia ulinzi na amani inaendelea kutawala.

 

Post a Comment

0 Comments