Akizungumza Juni 19, 2026, katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma, Afisa Mkaguzi wa Migodi wa Tume ya Madini, Rose Mika, amesema ukaguzi wa mara kwa mara unaofanyika katika migodi mikubwa, ya kati na midogo unalenga kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinaendeshwa kwa kuzingatia Sheria ya Madini pamoja na Kanuni za Usalama, Afya na Utunzaji wa Mazingira za mwaka 2010.
Amesema ukaguzi huo husaidia kubaini mapema changamoto zinazoweza kuhatarisha usalama wa wafanyakazi na wananchi wanaoishi jirani na maeneo ya migodi, hivyo kuwezesha hatua stahiki kuchukuliwa kabla ya kutokea kwa madhara.

Rose amesema Tume ya
Madini pia inaendelea kusimamia utekelezaji wa mipango ya usimamizi wa
mazingira, ikiwemo kudhibiti uchafuzi wa maji, hewa na ardhi pamoja na
kuhakikisha taka zinazotokana na shughuli za uchimbaji zinahifadhiwa na
kushughulikiwa kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.
Aidha,
amesema Tume inafuatilia utekelezaji wa mipango ya kufunga migodi (Mine
Closure Plans) ili kuhakikisha maeneo yaliyokwishafanyiwa uchimbaji
yanarejeshwa katika hali salama na yenye tija baada ya shughuli hizo
kukamilika.
Kwa mujibu wa Rose, hatua hiyo ni muhimu katika
kuhakikisha ukuaji wa sekta ya madini unaenda sambamba na uhifadhi wa
mazingira na ustawi wa jamii zinazozunguka maeneo ya migodi.
Mbali
na ukaguzi wa migodi, Tume ya Madini inaendelea kusimamia matumizi ya
baruti katika shughuli za uchimbaji, ikiwemo utengenezaji, uingizaji,
usafirishaji na biashara yake kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo.
Katika
Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Tume ya Madini inaendelea kutoa
elimu kwa wananchi na wadau kuhusu fursa mbalimbali zilizopo katika
sekta hiyo na kuwahamasisha kushiriki katika shughuli za utafiti,
uchimbaji, uchenjuaji, biashara ya madini pamoja na utoaji wa huduma
kwenye migodi ya madini kwa kuzingatia matakwa ya sheria, ili kuchangia
ukuaji wa uchumi wa Taifa. 

0 Comments