TRA YATAKIWA KUJIANDAA NA MABADILIKO YA KIUCHUMI NA KITECKNOLOJIA



Na Mwandishi wetu 
 
SERIKALI imeitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kujiandaa mapema kukabiliana na mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kiteknolojia yanayotarajiwa katika miaka 30 ijayo, ikieleza kuwa zaidi ya asilimia 70 ya shughuli za kiuchumi zitakuwa zikifanyika kwa njia za kidijitali.
 
Hayo ameyasema na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Nsubili Joshua, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omary, wakati wa Kongamano la Miaka 30 ya TRA tangu kuanzishwa kwake mwaka 1996, lililoandaliwa na TRA kupitia Chuo cha Kodi.

Joshua amesema  mabadiliko ya teknolojia yanayoendelea duniani yanahitaji TRA kuwa mbele ya wakati kwa kuandaa mifumo madhubuti ya usimamizi wa kodi itakayoweza kukusanya mapato kutoka biashara za mtandaoni na huduma zinazovuka mipaka ya nchi.

Amesema   pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 30 ya TRA, bado kuna haja ya kuimarisha mifumo ya kodi ili iendane na kasi ya maendeleo ya uchumi wa kidijitali unaotarajiwa kutawala katika miaka ijayo.

“Katika miaka 30 ijayo zaidi ya asilimia 70 ya shughuli za kiuchumi zitafanyika kwa njia za kidijitali hivyo TRA inapaswa kuwa tayari kuhakikisha mapato ya Serikali yanakusanywa kwa ufanisi bila kuathiri mazingira ya biashara na ubunifu,” amesema Joshua.

Alifafanua kuwa lengo la Serikali si kuzuia maendeleo ya teknolojia, bali kuhakikisha kunakuwa na usawa wa kodi na ulinzi wa mapato ya taifa huku mazingira bora ya uwekezaji na ushindani wa haki yakiendelea kudumishwa.

Aidha, aliitaka TRA kuongeza uwekezaji katika matumizi ya akili mnemba (AI), uchambuzi wa takwimu na mifumo ya ufuatiliaji wa miamala kwa wakati halisi ili kubaini mianya ya ukwepaji kodi na kuimarisha uwazi katika ukusanyaji wa mapato.

Joshua amesema matumizi ya teknolojia hizo yatasaidia kugundua udanganyifu mapema, kupunguza mawasiliano yasiyo ya lazima kati ya walipakodi na maafisa wa kodi pamoja na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma.



Pia aliitaka TRA kuendelea kubuni mifumo rahisi ya usajili, ukadiriaji na ulipaji kodi kwa sekta isiyo rasmi ikiwemo wafanyabiashara wadogo na wakulima, ili kupanua wigo wa walipakodi na kuongeza mapato ya ndani.

Amesema  mafanikio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 yatategemea kwa kiasi kikubwa uwezo wa nchi kukusanya mapato ya ndani na kuyasimamia kwa ufanisi, jambo linaloifanya TRA kuwa na jukumu muhimu katika safari ya maendeleo ya taifa.

Joshua amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya TRA, wafanyabiashara, watafiti na wadau wengine wa kodi ni muhimu katika kujenga mfumo wa kodi unaoendana na mahitaji ya uchumi wa kisasa na kuhakikisha Tanzania inanufaika kikamilifu na mapinduzi ya teknolojia yanayoendelea duniani.

 

Post a Comment

0 Comments