KITUO CHA UTALII IKOLOJIA SHINYANGA CHAZINDULIWA RASMI

 

                            Na Mwandishi wetu, Shinyanga

Shinyanga imepiga hatua mpya katika kukuza utalii wa mazingira baada ya kuzinduliwa rasmi Kituo cha Utalii Ikolojia (Ecotourism) katika Msitu wa Hifadhi wa Lubaga, mradi unaotarajiwa kuifanya hifadhi hiyo kuwa kivutio kipya cha utalii wa ndani, kuongeza ajira, kuimarisha uhifadhi wa mazingira na kuchochea uchumi wa wananchi kupitia matumizi endelevu ya rasilimali za misitu.

Uzinduzi huo umefanyika  tarehe 27 Juni , 2026 katika Msitu wa Hifadhi wa Lubaga uliopo Manispaa ya Shinyanga, ambapo Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga. Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa Serikali, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), wadau wa uhifadhi, sekta ya utalii pamoja na wananchi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Nkinda amesema tukio hilo si uzinduzi wa eneo la utalii pekee, bali ni hatua ya kuonyesha namna ambavyo rasilimali za asili zinaweza kubadilishwa kuwa fursa za maendeleo ya kiuchumi, ajira, elimu na burudani kwa jamii. 


Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, na viongozi mbalimbali wakifanya ziara ya kutembelea maeneo mbalimbali ya Msitu wa Hifadhi wa Lubaga na kujionea vivutio vya Utalii Ikolojia vilivyoanzishwa katika hifadhi hiyo.

Amesema kwa muda mrefu watu wengi wamekuwa wakihusisha utalii na mbuga za wanyama, milima na fukwe za bahari, lakini Msitu wa Hifadhi wa Lubaga unaonyesha kuwa hata Shinyanga ina hazina kubwa ya utalii wa mazingira inayostahili kutambulika, kuendelezwa na kutembelewa.

"Mkoa wa Shinyanga unaendelea kupiga hatua katika kuendeleza utalii wa ndani kwa kutumia rasilimali zilizopo. Hii ni fursa muhimu kwa wananchi wetu kujifunza kuwa utalii haupo mbali; unaweza kuanzia hapa hapa nyumbani kwetu," amesema Nkinda.

 Amesema utalii wa ndani una mchango mkubwa katika kuongeza mapato ya Serikali, kuibua fursa za biashara kwa jamii, kuhamasisha uhifadhi wa mazingira na kuimarisha utamaduni wa kuthamini urithi wa asili.

 

 

Post a Comment

0 Comments