Na Kareny Masasy, Kishapu
WATU 75 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoani Shinyanga kwa tuhuma ya kuhusika katika matukio mawili likiwemo la kuwashambulia watumishi wa serikali na kuchana nyaraka za serikali wakati wakiwa katika majukumu yao.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa Janeth Magomi amesema hayo huku akieleza sababu ya kushikiliwa watu hao ni kuwavamia na kuwashambulia watumishi watatu wa Kata ya Idukilo wakiwa kwenye majukumu yao kijiji cha Sanjo.
Kamanda Magomi amewataja walioshambuliwa ni Mtendaji wa Kata ya Idukilo Masembe Msele(50)Afisa maendeleo ya Jamii Kata ya Mwaduiluhumbo Rose Shao(38) walivamiwa na kupigwa.
Wengine ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Sanjo na kaimu mtendaji wa kijiji na wajumbe watatu wa serikali ya kijiji wakiwa kwenye zoezi la kuingiza kaya masikini kwenye mpango wa TASAF ambapo walivamiwa na watu waliokuwa na pikipiki mbili na kuanza kuwapiga.
Kamanda Magomi amesema watu hao walianza kuwapiga kisha kuchana nyaraka
ambazo walikuwa wameingiza baadhi ya majina kwenye mpango wa kaya masikini huku
wakidai hawataki kuona kiongozi yeyote wa serikali anafanya kazi ndani ya kata
hiyo.
Kamanda Magomi amesema kufuatia tukio hilo Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga lilianza upelelezi na kuwakamata watuhumiwa waliohusika na tukio hilo ambapo tukio jingine lilitokea Juni moja,2026 majira ya saa sita na nusu usiku katika Kijiji cha Idukilo baadhi ya wanakijiji walipigwa.
Magomi amesema tukio hilo wanakijiji hao wanadaiwa kupigwa kwa madai ya kuwa wao ndiyo wanatoa siri kwa Jeshi la polisi na Mkuu wa Wilaya kwa kupeleka majina ya wanaofanya fujo ambapo vurugu hizo zilisababisha uharibifu ikiwemo kuvunja baadhi ya maduka ya wafanyabiashara.
.jpg)
0 Comments