JENGO LA MAMA NA MTOTO ,MAABARA YA KISASA KUJENGWA HOSPITALI YA RUFAA SHINYANGA


Na Kareny  Masasy,Shinyanga

SERIKALI  kupitia Kampuni ya Ushauri Elekezi ya Volumetric Arch Consultant Ltd imekabidhi rasmi eneo la ujenzi wa Jengo la Mama na Mtoto la ghorofa tano pamoja na Jengo la Maabara ya Kisasa la ghorofa mbili yatakayo  gharimu shilingi bilioni 22 kwa mkandarasi atakaye tekeleza ujenzi huo

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo juzi katika eneo la hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga   Mshauri Mwelekezi wa Kampuni hiyo Berno Batinamani alisema  mradi huo unatarajiwa kuanza rasmi  mwezi Juni 19, 2026 na kukamilika mwaka 2028.

 Betinamani amesema  majengo hayo yatakapokamilika yataongeza uwezo wa hospitali kutoa huduma za kisasa za afya kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga na maeneo ya jirani.

 Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Tiba kutoka Wizara ya Afya ambaye pia ni Meneja wa Mkataba wa mradi huo Festo Mapunda alimtaka  mkandarasi kuhakikisha kazi inatekelezwa kwa ubora unaotakiwa na  kwa wakati uliopangwa kwa mujibu wa mkataba.

Mapunda alisisitiza pia  umuhimu wa kutumia nguvu kazi kutoka kwa wananchi wa ndani ya mkoa wa Shinyanga ili kuwawezesha kunufaika na fursa za ajira zitakazotokana na utekelezaji wa mradi huo.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Amar  Builders Ltd Mkandarasi anayejenga majengo hayo Vipul Maran amesema  kampuni yake imejipanga kikamilifu kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vyote vya kitaalamu vinavyohitajika.

Maran amesema  maandalizi ya awali ya utekelezaji wa mradi yamekamilika na kwamba wataendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali pamoja na mshauri mwelekezi ili kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa mafanikio

Akizungumza kwa niaba ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo Dkt. John Luzila alishukuru  Serikali ya awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya afya kupitia miradi mikubwa ya maendeleo inayolenga kuboresha huduma za matibabu nchini.

Dkt. Luzila amesema  Jengo la Mama na Mtoto litakuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa 162 kwa wakati mmoja hatua itakayosaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa na kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto katika mkoa huo

Dkt Luzila amesema  jengo jipya la maabara ya kisasa lenye ghorofa mbili litaboresha huduma za uchunguzi na vipimo mbalimbali vya kitabibu hivyo kuwawezesha wananchi kupata huduma nyingi za vipimo katika eneo moja bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo.


 

Post a Comment

0 Comments