WANANCHI ISAKA WASHIRIKI UJENZI WA KITUO CHA POLISI




 WANANCHI wa kata ya Isaka Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama  mkoani Shinyanga kwa kushirikiana na jeshi la polisi, wamejitolea kujenga kituo cha polisi kilichogharimu  Shilingi Milioni 236 huku wananchi wakichangia Shilingi  Milioni 6.8,vifaa pamoja na nguvu kazi.

Akizungumza  wakati wa uzinduzi wa kituo hicho kamanda wa polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi aliwashukuru  wananchi wa Isaka kwa hatua hiyo na kuahidi kuimarisha hali ya usalama katika eneo hilo.






Kamanda Magomi amewasihi wananchi wa Isaka kukitumia kituo hicho kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu, na kwamba jeshi hilo litaficha siri ya kila mtoa taarifa kwa usalama wake.

"Jeshi la polisi tutahakikisha Isaka na maeneo mengine yanakuwa salama wakati wote kutokana na shughuli zilizopo hapa niwaombe wananchi tumieni kituo hiki tuleteeni taarifa za uhalifu na wahalifu.”amesema Magomi.

Mkuu wa polisi wilaya ya kipolisi Msalala (OCD), Yahya Shabani amesema  katika awamu ya kwanza wananchi walichangia nguvu kazi pamoja na fedha Shilingi Milioni 26 na zilizokamilisha hatua ya boma.

 “Mradi huu wa kituo cha polisi Isaka uliendeshwa kwa uratibu wa nguvu za wananchi kutokana na kukua kwa mji   huu na uwepo wa bandari kavu na mwingiliano mkubwa wa watu  na kibiashara.”amesema  Shabani.
Mbunge wa Msalala, Mabula Magangila, amesema kuimarika kwa ulinzi na usalama kutasaidia kuchochea ukuaji wa uchumi katika eneo hilo  hasa kutokana na ongezeko linalotarajiwa la magari makubwa yanayofika katika eneo la bandari kavu.

“Isaka ni miongoni mwa bandari kavu kongwe hapa nchini kuliko bandari zote, na inahudumia nchi nyingi kuliko bandari nyingine yoyote ile. Nchi zote za maziwa makuu baada ya kukamilika SGR zitachukulia mizigo yake hapa, hakuna namna ni lazima usalama uimarishwe.” amesema  Magangila.

 "


Post a Comment

0 Comments