WANANCHI WASHAURI KUCHIMBIWA KISIMA WAKISUBIRI MRADI WA ZIWA VICTORIA


 Na  Kareny Masasy,Shinyanga

WANANCHI wa  kata ya Usanda Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wameomba kuondolewa kero ya ukosefu wa maji safi kwa  kuchimbiwa kisima wakati wakisubiri utekelezaji wa mradi wa maji safi kutoka ziwa victoria.

Wananchi hao  wameongea mbele ya  Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro   kwenye mkutano wa  uendeshaji wa kliniki ya utatuzi wa kero mbalimbali zinazowakabili wananchi  iliyoanza rasmi kwenye tarafa ya Samuye.

Mkazi wa Kata ya Usanda George Shija ameeleza  kuwa kero hiyo imekuwa kwa muda mrefu na kwa muda mwingine wakazi wa mbali na mto  Shimiu wamekuwa wakiuziwa maji  kwa shilingi 100 kutoka  kwenye mto huo.

“Changamoto yangu ni maji ya mto tunayotumia si salama, nakero ya maji katika eneo hili imekuwepo kwa muda mrefu hatuna maji safi na salama, pia maji haya haya tunakunywa na kuchangia na mifugo”amesema Shija.

Pia mkazi wa kata hiyo Samweli Mhama ameeleza   kuna muda maji katika mto  huo yanaisha kwa kukauka   japo si salama lakini wanachimba mpaka kina cha mto ili kupata ya kutumia na changamoto hii niya miaka mingi sasa.

Mfanyabiashara ya maji  kutoka kijiji hicho  Thomas Ngassa amesema kwa sasa wanauza maji haya ya mtoni kwa dumu tano za lita 20 bei  yake shilingi  1,500  ikifika kipindi cha mwezi Julai  wanapandisha na kuuza shilingi 2000.

Meneja wa Wakala wa maji  na usafi wa  Mazingira vijijini  (Ruwasa) wilaya ya Shinyanga  Mhandisi Emmael Mkopi amesema   kwa sasa wanafanya tathimini ya ujenzi wa tanki la maji ya ziwa Victoria na wako katika hatua za mwisho kukabidhi mradi.

“ Tenki la maji litajengwa  lenye ujazo wa lita 1,150,000 na wananchi watanufaika  na katika suala la uchimbaji wa kisima tunalifanyia kazi pia ” amesema  Mhandisi  Mkopi.


Post a Comment

0 Comments