BAADHI ya wakazi wa kijiji cha Singita kata ya Usanda
halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa huduma
za maji, hali inayowalazimu kwenda kuchota maji mto Shimiwi huku wakihofia afya
zao kukumbwa na magonjwa ya mlipuko pia kuchangia na mifugo.
Hayo yalielezwa na baadhi ya wananchi wakati wakizungumza na
waandishi wa habari waliotembelea kijijini humo,ambapo walisema hakuna visima
vya maji wala mabomba na kwamba maji wanayotumia wanakwenda kuchimba
mtoni na wakati mwingine hukuta fisi wakinywa maji.
Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti baadhi ya
wananchi hao Rehema Samson,Maria Maige na Peter Nkilijiwa,walisema kilio chao
wameshakifikisha kwa mbunge wa jimbo la Solwa Ahamed Salum na
diwani wakata hiyo Abeid Aljabiri lakini bado ufumbuzi haujapatikana.
“Shida ya maji ipo hakuna mpaka tufuate mtoni au kununua dumu
shilingi 200 na wakati mwingine inafika mpaka 300 kutegemeana na umbali
unaokaa,kwa kweli ndugu mwandishi tunateseka tufikishieni kilio chetu kwa
serikali tumekuwa kama watoto yatima hatuna msaada”alisema Maria Maige.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kijiji hicho Mohamed Jumanne,alisema kuna
vitongoji 10 lakini vyote havina huduma ya maji ya kuridhisha, ambapo ameiomba
serikali kusikia kilio chao na kuwapatia msaada wa haraka kwa kuwachimbia
visima ili waondokane na kero hiyo.
Mwenyekiti huyo alisema ,hali huwa mbaya zaidi wakati wa kiangazi kwa
kuwa maji hukauka mtoni, hivyo wananchi huchimba kwa kufuata mkondo wa
mto ili wapate maji jambo ambalo linaweza kuhatarisha maisha yao kwa kufukiwa
na udongo unaokuwa umerundikwa kwa kuwa wanakuwa ndani ya shimo.
Naye diwani wa kata hiyo Abeid Aljabiri akitoa ufafanuzi wa tatizo hilo
alisema,halmashauri ilitoa ahadi ya kuwachimbia visima vitatu na tayari
wameshatembelea maeneo yanayofaa lakini mpaka sasa hakuna utekelezaji na pindi
anapofuatiliahakuna jibu la moja kwa moja linalotolewa juu ya huduma ya maji.
Alisema pia tatizo jingine ni ucheleweshaji wa fedha za shughuli za maendeleo
kutokufika kwa wakati na kuomba ngazi za juu kupitia kwa waziri husika kufika
Usanda kujionea kero hiyo kwani hata mtandao wa maji ya ziwa victoria
wamesahaulika na badala yake kata za jirani zimewekwa Samuye,Mwantini na Tinde.
0 Comments