Na Mwandishi wetu,
Himofilia
ni ugonjwa wa kurithi wa damu unaosababisha mwili kushindwa kugandisha
damu kwa kawaida kutokana na upungufu wa vinasaba vya kugandisha damu
(clotting factors).
Hali hii hupelekea damu kuvuja kwa muda mrefu kuliko kawaida au kutokwa damu ndani ya mwili.
Hata hivyo, takribani asilimia 30 ya wagonjwa hupata himofilia bila kurithi (sporadic hemophilia), hali inayotokana na mabadiliko ya vinasaba (gene mutation) yanayotokea bila historia ya ugonjwa katika familia.
Mtu mwenye himofilia huishi na ugonjwa huu maisha yake yote, kwani hauponi kabisa, lakini unaweza kudhibitiwa kwa matibabu sahihi na ya mara kwa mara ili kuzuia madhara makubwa.
Dalili za himofilia ni pamoja na kutokwa na damu ndani ya mwili bila jeraha la wazi, hasa kwenye ubongo, misuli au maungio, pamoja na kuvimba na maumivu kwenye viungo kutokana na damu kuvuja ndani. Vilevile, mgonjwa anaweza kupata kutokwa na damu kwa muda mrefu isivyo kawaida baada ya kupata jeraha, pamoja na kutokwa na damu nyingi baada ya kufanyiwa upasuaji au kung’olewa jino.


0 Comments