SHUWASA KUJA NA MPANGO WA MALIPO YA KABLA KUONDOA CHANGAMOTO


Na Kareny Masasy,
Shinyanga

MAMLAKA ya maji safi na usafi wa mazingira Shinyanga (Shuwasa) imekuja na mpango wa kutumia mita za malipo ya kabla(Prepaid meters) hatua inayolenga  kuondoa changamoto ya ulipaji wa bili hasa kwenye vituo vya umma vya kuchotea maji ili kuongeza uwajibikaji kwa watumiaji.

Akizungumza katika mkutano wa wadau wa maji safi   wa kupitia rasmu ya mkataba wa huduma kwa mteja ,Mkurugenzi wa Shuwasa Mhandisi Yusuph Katopola amesema  kufunga mita za maji za malipo ya kabla kwenye maghati itawawezesha kuondoa usumbufu .

Katopola amesema  kuwa katika awamu ya kwanza zoezi hilo litaanza mwezi Aprili  kutekelezwa kwenye maeneo yenye changamoto kubwa ya ulipaji wa bili, hususan kwa wateja wanaoshindwa kulipa kwa wakati au wanaolimbikiza madeni ambao wanahudumiwa na Mamlaka hiyo.

“Tunajenga magati ya maji ili kusaidia Jamii ya eneo hilo maana unapotekeleza mradi ukishakamilika halafu wananchi wakakosa huduma mpaka wasubiri kuunganishiwa inakuwa vigumu na ndiyo maana tunaweka maghati kusaidia Jamii”amesema  Katopola Mhandisi  Katopola

 Mhandisi Katopola amesema  mkataba wa zamani umeisha muda wake, na mamlaka hiyo iko katika hatua za mwisho za kukamilisha rasimu ya mkataba mpya utakaodumu kwa miaka mitatu kuanzia 2026 hadi 2029 baada ya kupitishwa na Ewura.

Wadau wa sekta ya maji akiwemo Anascholastika Ndagiwe wamepongeza  Shuwasa kwa ubunifu huo, wakieleza kuwa ni suluhisho la kudumu litakalosaidia kuboresha huduma ya maji na kuongeza nidhamu ya matumizi kwa wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga  Julius Mtatiro ametoa  wito kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga  kuzingatia kikamilifu mkataba wa huduma kwa mteja pamoja na miongozo ya kisheria ili kuboresha utoaji wa huduma .

Amesisitiza suala la kufanya kazi kwa weledi na kutoa huduma bora kwa wananchi wa Manispaa ya Shinyanga, huku akitaka kero zinazowakabili watumiaji wa maji kutatuliwa kwa haraka na kwa ufanisi.


 

Post a Comment

0 Comments