MANISPAA ya
Kahama Mkoani Shinyanga inatarajia kupokea
wanafunzi 25,113 watakao anza kidato cha kwanza mwaka 2027 huku ikiwa na upungufu wa vyumba vya madarasa 246
na matundu ya vyoo 536.
ofisa elimu sekondari Manispaa hiyo Anastazia Vicent amesema hayo leo kwenye kikao cha baraza la madiwani cha robo ya kwanza ya mwaka 2026/2027 ambapo aliwaelewa madiwani inahitajika ushirikiano wakutosha kuweza kutatua changamoto ya upungufu uliopo.
Anastazia amesema kuna mahitaji ya jumla ya vyumba vya madarasa 502 vilivyopo ni 256 na upungufu ni 246 na pia kuna upungufu wa matundu ya vyoo 536 na viti na meza 16,839 na maabara 26.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama Masudi Kibetu amesema baadhi ya kata wameanza utekelezaji ujenzi wa vyumba vya madarasa na sasa wanakwenda kuainisha kwenye kila kata kujengwe vyumba vya madarasa vipya au shule na matundu ya vyoo yanayohitajika.
Katibu tawala wilaya ya Kahama Glory Absalum amesema idadi hiyo ya wanafunzi kwa mwezi Januari mwakani wanatakiwa waingie darasani na watapita kila kata kuona hatua zilizofanyika au kufikiwa ili kuondoa changamoto ya upungufu huo.
“Madiwani niwaombe muendelee kutoa elimu kwa wazazi huko mliko wasiwaache watoto watembee kwenye madimbwi shule zimefungwa sasa mvua hazitabiliki zisiweze kuwaletea madhara”amesema Glory.
Katibu tawala Msaidizi kutoka ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Adonias Nyamjulirwa amesema halmashauri hii iendelee kujikita katika ukusanyaji wa mapato ya ndani nakufikia malengo yaliyokusudiwa ili kuondoa mapungufu yaliyopo kwa wanafunzi.
“Zinahitajika shilingi bilioni 5.8 za mapato ya ndani kuweza kukamilisha mapungufu yote yaliyotajwa na ofisa elimu sekondari ndani ya siku zilizobaki ili wanafunzi wasipate changamoto katika elimu wanayoitafuta”amesema Nyamjulirwa.
Mwisho




0 Comments