Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Mhe. Peter Masindi, amewapongeza wahitimu wa mafunzo ya awali ya Jeshi la Akiba, intake ya 53, na kuwataka kutumia ujuzi walioupata kulinda amani, kudumisha uzalendo, kuimarisha nidhamu na kushiriki katika shughuli za maendeleo ya jamii.
Masindi ameyasema hayo Oktoba 29, 2026, wakati akifunga mafunzo hayo yaliyofanyika katika viwanja vya Shirecu wilayani Kishapu, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kulitumia Jeshi la Akiba katika kazi maalumu za kiusalama, ikiwemo kusaidia ulinzi wa taasisi mbalimbali kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.

“Nawapongeza kwa kuhitimu mafunzo haya na kufungua ukurasa mpya wa kulitumikia taifa. Kupata cheti cha Jeshi la Akiba ni hatua muhimu, lakini jambo kubwa zaidi ni namna mtakavyotumia maarifa na ujuzi mlioupata. Nendeni mkaitumikie jamii kwa uadilifu, nidhamu na uzalendo, na muwe sehemu ya kulinda amani na usalama wa nchi yetu,” amesema Masindi.


Amesisitiza kuwa wahitimu wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa katika jamii kwa kuheshimu sheria, kufuata maelekezo halali, kulinda mali za umma na binafsi, kutoa taarifa za viashiria vya uhalifu kwa vyombo husika na kushirikiana na wananchi wengine katika kuzuia vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani na usalama.


Amesema Jeshi la Akiba lina nafasi muhimu katika kuimarisha ulinzi na usalama nchini, hususan linaposhirikiana na Jeshi la Polisi na vyombo vingine vinavyohusika, huku akiwataka wahitimu kutotumia ujuzi walioupata kuwatisha, kuwaonea au kuwanyanyasa wananchi.


“Mnapaswa kuelewa kuwa mafunzo haya yamewajengea uwezo wa kulitumikia taifa na kusaidia jamii. Nidhamu, uvumilivu na utii kwa sheria viwe sehemu ya maisha yenu ya kila siku. Msiwe chanzo cha migogoro, bali muwe watu wa kuleta suluhu, mshikamano na maendeleo katika maeneo mnayoishi,” amesisitiza.




Kwa upande wake, Kaimu Mshauri wa Jeshi la Akiba, Kapteni Ms. Mhina, amewashukuru wahitimu kwa kukamilisha mafunzo hayo na kupongeza ushirikiano uliotolewa na uongozi wa Wilaya ya Kishapu pamoja na wadau wengine katika kufanikisha mafunzo hayo.


Mhina ameeleza kuwa mafunzo ya Jeshi la Akiba yana umuhimu mkubwa katika kuwajengea washiriki uwezo wa kutekeleza majukumu ya kiusalama, kukabiliana na majanga, kuimarisha uzalendo na kujenga uelewa wa masuala mbalimbali yanayohusu ulinzi wa taifa.


Akisoma risala ya wahitimu, MGM Suzan Joseph, akishirikiana na MG. Renatus Tinde, amesema mafunzo hayo yaliyoanza Julai 1, 2026 na kufungwa Oktoba 29, 2026, yamewajengea washiriki uwezo wa kufuata maelekezo, utii na nidhamu, kuimarisha usalama wa nchi, kuongeza uimara wa mwili na akili, kukabiliana na kuzuia majanga pamoja na kujifunza masuala ya ujasiriamali na matumizi bora ya rasilimali.


Hata hivyo, risala hiyo imeainisha changamoto zinazohitaji kupewa kipaumbele, ikiwemo upungufu wa fedha za kuboresha mazingira ya kujifunzia na vifaa muhimu vya mafunzo kama sare za kombati na buti. Changamoto nyingine ni uhaba wa maeneo maalumu ya kufanyia mafunzo, hali inayosababisha baadhi ya mafunzo kufanyika karibu na makazi ya wananchi, pamoja na uelewa mdogo wa baadhi ya wananchi kuhusu madhumuni ya mafunzo hayo.


Wahitimu wameiomba Serikali na uongozi husika kuendelea kuboresha mazingira ya mafunzo, upatikanaji wa vifaa na elimu kwa wananchi ili kuongeza uelewa kuhusu nafasi ya Jeshi la Akiba katika kulinda taifa na kusaidia jamii.


Jumla ya wahitimu waliojiandikisha hapo awali walikuwa 75  na waliohitimu leo kuwa ni 64 wanaume 57 na wakike 7 huku wengine 11 wakiishia njian kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na utovu wa nidhamu.


Mafunzo ya awali ya Jeshi la Akiba yana mchango muhimu katika kujenga vijana wenye nidhamu, uzalendo, utii na uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali. Mbali na kuwapa ujuzi wa masuala ya ulinzi na usalama, mafunzo hayo yanawajengea uwezo wa kujitegemea, kukabiliana na majanga na kushiriki katika shughuli za maendeleo, huku yakipanua wigo wa vijana kushiriki katika kulinda amani na usalama wa nchi.

Post a Comment

0 Comments