MFUKO wa Mafao kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umeendelea kuboresha mifumo yake kwa kuendana na usawa wa kidijitali ikiwa lengo pia kuwarahisishia watumishi waliostaafu kupata huduma kwa ukaribu bila kuwa na vikwazo vyovyote ikiwemo kusafiri kupata huduma ofisini.
Hayo yameelezwa leo na wawezeshaji kutoka PSSSF ambao wameandaa semina hiyo kwa waandishi wa habari kutoka Mtandao wa Wanablogu Tanzania ( TBN) na Klabu za Waandishi wa Habari za mikoa ya Shinyanga na Simiyu kwaajili ya kufahamu vyema mfuko huo nakuhabarisha kwa usahihi uliopo.
Hata hivyo kupitia mafunzo yaliyotolewa waandishi wa habari wameshauriwa kutumia taaluma zao kuwaelimisha na kuwahamasisha wanachama kuhakiki taarifa za michango na mafao yao kupitia mifumo ya kidijitali.
Kaimu Afisa Mfawidhi PSSSF Shinyanga Sunday Rashid, amesema mfuko umeanza kushughulikia taarifa za watumishi wanaokaribia kustaafu miezi sita kabla ya tarehe yao rasmi ya kustaafu ili kutoa muda wa kuhakiki taarifa na kurekebisha changamoto zao
Msimamizi wa mfuko wa PSSSF Mkoa wa Simiyu Salum Miraji ameeleza matumizi ya mifumo ya kidijitali yamekuwa sehemu ya maboresho ya huduma za mfuko, yakilenga kumwezesha mwanachama kupata na kuhakiki taarifa zake bila kulazimika kufika ofisini.
Miraji ameeleza kuwa mwanachama anaweza kutumia mfumo huo kufuatilia taarifa zake, ikiwemo taarifa za michango, na kubaini mapema endapo kuna taarifa zisizo sahihi ambazo zinaweza kuleta changamoto wakati wa uchakataji wa mafao yake.
Mratibu wa Tanzania Bloggers Network – TBN Kanda ya Ziwa, Kadama Malunde, amesisitiza umuhimu wa waandishi kutumia nafasi yao na taaluma waliyonayo kuwafikishia wananchi elimu na taarifa sahihi zinazoweza kuwasaidia kutambua haki na huduma wanazostahili.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa TBN, Beda Msimbe, Malunde amesema waandishi wana nafasi muhimu katika kuhakikisha wananchi wanaelewa masuala ya hifadhi ya jamii, ikiwemo umuhimu wa wanachama kufuatilia taarifa zao za michango na mafao kwa kutumia mifumo inayotolewa na taasisi husika.
Malunde amesema mafunzo wanayopata waandishi yanapaswa kuwa chachu ya kuongeza uelewa wao na baadaye kutumia ujuzi huo kuwaelimisha wananchi kwa lugha rahisi, sahihi na inayoeleweka.
“Leo tunapaswa kuwa na furaha ya kupata elimu. Kwa mwandishi wa habari, kujifunza ni sehemu ya kazi yetu. Dunia inabadilika, teknolojia inabadilika na mahitaji ya jamii yanabadilika,” amesema Malunde.
Malunde amesema TBN, iliyoanzishwa mwaka 2015, imeendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali, ikiwemo PSSSF, katika mafunzo na ujenzi wa uwezo wa wanablogu na watengeneza maudhui nchini.
Amesema maendeleo ya teknolojia yameongeza kasi ya usambazaji wa taarifa, hivyo waandishi wanapaswa kuwa makini kuhakikisha taarifa wanazozifikisha kwa jamii zinathibitishwa, zina usahihi na zinazingatia misingi ya uwajibikaji wa taaluma.





0 Comments