WAFANYABIASHARA,MAKAMPUNI NA TAASISI MKOANI SHINYANGA WATAKIWA KUENDELEA KULIPA KODI


Na  Mwandishi wetu , Shinyanga 

KATIBU Tawala wa Mkoa wa Shinyanga  Salum Hamduni, amewataka wafanyabiashara, makampuni na taasisi mbalimbali mkoani humo kuendelea kulipa kodi kwa hiari, kwa usahihi na kwa wakati pasipo kukwepa wala udanganyifu  ili kuiwezesha Serikali kupata rasilimali za kutekeleza miradi ya maendeleo.

Hamduni amezungumza hayo  katika kilele cha maadhimisho ya miaka 30 ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Shinyanga yaliyofanyika katika Ukumbi wa Level One, Manispaa ya Shinyanga, ambapo ameanisha kuwa  maendeleo makubwa yanayoonekana nchini, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara na kuboreshwa kwa huduma za kijamii, yanatokana na mapato yanayokusanywa kupitia kodi.

Amesema ni wajibu wa kila mlipa kodi kutimiza wajibu wake kwa hiari ili kuendelea kuimarisha uchumi wa taifa na kuongeza uwezo wa Serikali wa kutoa huduma kwa wananchi kwani TRA imeendelea kusimamia majukumu yake ya ukusanyaji kodi na mapato mengine ya serikali  kwa mujibu wa sheria.

 Hamduni ameongeza kuwa TRA imeendelea kuwezesha ulipaji wa kodi kwa hiari pamoja na kuchangia maendeleo endelevu  ya kijamii na kiuchumi katika taifa la Tanzania huku akiwapongeza watumishi wa mamlaka hiyo kwa kufanya kazi kwa weledi,ufanisi  na uwazi hali iliyopelekea  ongezeko la makusanyo mwaka kwa mwaka

“ Tumeshuhudia maendeleo makubwa sana katika utoaji wa huduma za jamii,tumeshuhudia kujengwa kwa shule nyingi,  hii yote inatokana na ukweli kwamba watanzania sasa wanatambua na wamejitoa katika suala zima la ulipaji kodi”amesema  Salum Hamduni

 Katika hatua nyingine  Hamduni amewata  watumishi wa mamlaka  ya mapato Tanzania   mkoa wa Shinyanga  kuendelea kutoa huduma bora kwa kuzingatia uadilifu, uwazi na weledi ili kujenga na kuimarisha imani ya walipa kodi kwa mamlaka hiyo.

 Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Shinyanga, Ramadhan Sengo, amesema  katika kipindi cha miaka 30 tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo, kumepatikana mafanikio makubwa hasa baada ya kuanza kujiendesha kisasa na  kidigitali.

Amesema  TRA pia imeboresha miundombinu ya ofisi na huduma zake, hatua iliyochangia kuongezeka kwa makusanyo ya kodi na kuwezesha Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.

Nao baadhi ya wadau na walipa kodi waliojitokeza katika hafla hiyo akiwemo Hulda Gambago ambaye ni mshauri wa wawalipa kodi amesema miaka 30 ya TRA imekuwa na mafanikio kwani  kumekuwa na uwazi katika suala la ukusanyaji wa mapato, tofauti na miaka ya nyuma huku Ancy Stanslaus na Khalid Shabani ambao ni maafisa usafrishaji maarufu kama bodaboda  wakiwashi watanzania kuendelea kulipa kodi.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ni taasisi ya Serikali iliyoanzishwa mwaka 1995 na kuanza rasmi shughuli zake tarehe 1 Julai 1996. Jukumu lake kuu ni kusimamia ukusanyaji wa kodi na mapato mengine ya Serikali Kuu kwa ufanisi na kwa mujibu wa sheria.

  

Post a Comment

0 Comments