MRADI WA EACOP WAFIKIA ASILIMIA 86 NAKUTARAJIA KUSAFIRISHA MAFUTA GHAFI

                     

Na  Mwandishi wetu, Tanga 

WAZIRI wa Nishati, Dkt. Deogratius Ndejembi, amesema ujenzi wa Mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) umefikia asilimia 86, huku mafuta ya kwanza yakitarajiwa kupokelewa katika Kituo cha Chongoleani, Tanga, na kusafirishwa Januari mwaka 2027.
Dkt. Ndejembi alisema hayo leo baada ya kutembelea eneo la mradi Chongoleani, mkoani Tanga, kujionea maendeleo ya utekelezaji wake, ambapo alieleza kuwa matarajio ni kukamilisha ujenzi huo ifikapo mwisho wa Agosti mwaka huu.

Amesema  kazi nyingi muhimu zimekamilika na kilichobaki ni hatua za mwisho ikiwemo kukamilisha miundombinu ya umeme ili kuwezesha mitambo ya kusukuma mafuta kufanya kazi.

"Nimefurahishwa na maendeleo ya mradi. Kazi kubwa imefanyika na tunaamini ifikapo mwisho wa Agosti ujenzi utakuwa umekamilika. Ratiba inaonyesha kuwa meli ya kwanza itachukua mafuta ghafi kutoka Chongoleani mwezi Januari, 2027," amesema.

Hata hivyo, amesema  changamoto iliyobaki ni kukamilika kwa njia ya umeme kutoka Majani Mapana kuelekea eneo la mradi, huku akiutaka mkandarasi anayetekeleza kazi hiyo chini ya Tanesco kuhakikisha anakamilisha mradi huo kwa wakati.

Alionya kuwa mkandarasi atakayeshindwa kutekeleza kazi hiyo ndani ya muda uliopangwa atachukuliwa hatua, ikiwemo kuondolewa katika orodha ya wakandarasi wanaofanya kazi na Tanesco.

Dkt. Ndejembi amesema  EACOP ni mradi wa kimkakati kwa Tanzania, Uganda na ukanda mzima wa Afrika Mashariki, akibainisha kuwa bomba hilo lenye urefu wa zaidi ya kilomita 1,400 ni la kwanza duniani lenye mfumo wa kupashwa joto katika urefu wake wote.

Amesema  Serikali ya Tanzania imewekeza zaidi ya Sh bilioni 973 kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), ambalo linamiliki asilimia 15 ya hisa za mradi huo kwa kushirikiana na kampuni za UNOC, TotalEnergies na CNOOC.

Aidha, amewataka  Watanzania kuendelea kutumia fursa zinazotokana na mradi huo, akieleza kuwa zaidi ya Watanzania 3,000 wamepata ajira za moja kwa moja, huku vijana wengine zaidi ya 100 wakipelekwa Madimba kwa mafunzo ya kuongeza ujuzi kabla ya kuajiriwa.

Aliongeza kuwa zaidi ya vijana 400 kutoka Chongoleani wamepatiwa mafunzo na kuajiriwa katika maeneo mbalimbali ya mradi huo, huku fursa nyingine nyingi zikiendelea kujitokeza.

Post a Comment

0 Comments