ZAIDI ya abiria 60 wamenusurika kufa huku majeruhi wakiwa 52 baada ya
basi la Supernajimunisa lenye namba za usajili T.242 BRJ walilokuwa
wanasafiria kutoka Jijini Mwanza kuelekea jijini Dar es salaam kupinduka
katika kijiji cha Busanda kata ya Usanda mkoani Shinyanga.
Ajali
hiyo imetokea leo majira ya saa tatu asubuhi ambapo basi hilo aina ya
scania mali ya kampuni ya Supernajimunisa likitokea Mwanza kuelekea Dar
es salaam likiwa na idadi ya abiria hao ambapo lilipasuka tairi la
mbele kulia na kupinduka. ikiwa majeruhi katika ajali hiyo walikimbizwa
katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya matibabu kwani
wengine hali zao zilikuwa mbaya.
Akizungumza na mwandishi wa
habari hizi mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt Ntuli Kapologwe
alisema hospitali ya mkoa wa Shinyanga imepokea majeruhi 52 ambapo kati
yao majeruhi waliolazwa ni 22,ambao wanne kati yao hali zao ni mbaya
ambao ni wanaume wawili na wanawake wawili.
Dkt Kapologwe
alisema kuwa kati ya majeruhi hao waliopokelewa katika hospitali hiyo
tayari majeruhi 30 wamesharuhusiwa kutoka hospitalini hapo.
Hata
hivyo baadhi ya majeruhi waliolazwa katika hospitali hiyo walisema
ajali hiyo ilitokea baada ya tairi la mbele la basi hilo kupasuka na
kusababisha basi kuingia mtaroni na kujeruhi abiria waliokuwa ndani ya
basi.
“Mwendo wa basi ulikuwa wa kawaida,tairi lilichomoka gari
likapinduka ,kama lingekuwa katika mwendo kasi naamini lazima watu
wangekufa,lakini hakuna aliyekufa katika ajali hii”,alisema Daudi
Mapunda aliyekuwa anasafiri kutoka Mwanza kwenda Dar es salaam.
Kwa
upande wake Edina Shija ambaye ameumia kidevuni alisema basi lilikuwa
katika mwendo wa kawaida huku akiwataka wahusika wa magari kujenga tabia
ya kukagua vizuri vyombo vya usafiri ili kuepuka ajali zisizokuwa za
lazima.
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa uchunguzi wa awali
unaonesha kwamba pamoja na kupasuka kwa tairi basi hilo lilikuwa katika
mwendo kasi huku uchunguzi ukiendelea.
0 Comments