.
BAADHI ya wazazi na walezi
manispaa ya Shinyanga asilimia kubwa wamekuwa hawapendi kuchangia
miradi ya maendeleo mbalimbali ikiwemo sekta ya elimu hali ambayo
imeonyesha katika shule ya sekondari Mazinge kushindwa kuchangia
huduma ya wanafunzi kupata uji na chakula cha mchana.
Ikiwa kila
mwanafunzi inatakiwa achangie kiasi cha shilingi 3000, hivyo Idadi ya
wanafunzi waliotoa michango yao ni 6 pekee kwa shule nzima kati ya
wanafunzi 664 kwa lengo la kupata uji wawapo shuleni hapo, imeelezwa
wazazi ndio chanzo cha kudhorotesha kutokupata huduma hiyo ikiwa katika
sherehe za harusi wanakuwa mstari wa kwanza kuchangia.
Diwani
wa kata ya Ndembezi katika manispaa ya Shinyanga David Nkulila,ambaye
pia ni naibu meya wa manispaa hiyo aliyasema hayo wakati wa kikao cha
kamati ya maendeleo ya kata hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi
ya afisa mtendaji wa kata hiyo.
Nkulila alisema hayo baada ya
kupewa taarifa na mkuu wa shule ya sekondari Mazinge iliyopo katika kata
hiyo,kuhusu mchango kwa ajili ya wanafunz 664,ambapo kati ya hao 6
pekee wamechanga huduma ya uji tangu mwaka jana.
Nkulila alisema
ni vyema sasa wananchi wakabadilika na kuona umuhimu wa kujali watoto
kwamba tatizo siyo wananchi kukosa elimu bali kinachotakiwa ni wananchi
kupewa hamasa na viongozi kuwa mstari wa mbele kuchangia.
“Wananchi
wanahitaji hamasa siyo elimu,na katika hili sisi viongozi tunapaswa
kuwa wa kwanza kuchangia hata kama hatuna watoto katika shule,mimi
nilichangia magunia ya mahindi katika shule za kata hii,na nimetoa
gunia la mchele katika shule ya sekondari Mazinge”,aliongeza Nkulila.
Naye mkuu wa shule ya sekondari Mazinge Henry Ntuah alisema sababu
zinazopelekea wananchi kuwa nyuma kuchangia elimu mfano huduma ya
chakula kwa wanafunzi ni wazazi na walezi kutohudhuria vikao vya shule
pindi wanapohitajika.
Ntuah alisema wazazi wanaohudhuria vikao
vya shule ni wachache matokeo yake utekelezaji wa mpango wa chakula kwa
wanafunzi ikiwa ni agizo la mkuu mkoa wa Shinyanga kwa kila shule kupata
huduma ya chakula na uji unakwama.
Nao wajumbe wa kamati hiyo
mbali na kumpongeza diwani wa kata hiyo kuwa mstari wa mbele kuchangia
sekta ya elimu katika kata yake ,ambapo mratbu elimu kata Seleman Bulugu
alisema kuwa diwani aliweza kutoa michango ya magunia kumi na moja
kwaajili ya shule tatu za msingi zilizopo kwenye kata huku wakitaka
viongozi wengine kuiga mfano wake.
0 Comments